Translate

Tuesday, March 26, 2013

PRESS RELEASE BY THE UNITED CHRISTIANS OF NZEGA TABORA OVER THE SUPPRESSION BY GOVERNMENT OF TANZANIA


UMOJA WA MADHEHEBU YA KIKRISTO WILAYA YA NZEGA.



OFISI YA UMOJA WA MADHEHEBU



S.L.P 245,



NZEGA.






Kumb Na. UMKN/03/2013/011 20/03/2013






MKUU WA MKOA,

S. L. P 25,

TABORA.



YAH: TAMKO LA UMOJA WA MAKANISA WILAYA YA NZEGA (TEC, CCT, PCT) KUHUSU MWENENDO NA VITENDO VYA SERIKALI NA MAMLAKA ZA

WILAYA DHIDI YA KANISA.

UTANGULIZI:

Sisi viongozi wa Umoja wa Madhehebu ya Kikristo Wilaya ya Nzega (UMKN) yakiwemo Makanisa ya TEC, CCT, PCT ya Wilaya ya Nzega tunaloliongoza kwa pamoja, tumekuwa wenye furaha wakati wote kwa amani, mshikamano na Umoja ambao umekuwepo kati yetu na Jamii zote za watu Wilayani mwetu na Taifa kwa ujumla. Tumefurahia pia ushirikiano mkubwa baina yetu na Serikali ya Wilaya na ile Serikali Kuu iliyopewa Mamlaka na Mungu ya kuongoza Taifa letu. Tunaamini kuwa Mungu ndiye aliyetupa Neema hii ambayo watu wa Jamii nyingi duniani wameikosa.

Kwa muda mrefu sasa Serikali Kuu pamoja na Serikali ya Wilaya yetu ya Nzega imejijengea heshima kati ya Waumini wa Madhehebu mbalimbali na wale wasio na dini kwani imetenda mambo yake kwa Utawala wa Sheria. Aidha tunatambua kuwa Tanzania, Nzega ikiwa sehemu yake, ni Nchi inayofuata Utawala wa Sheria unaothamini haki za binadamu na misingi ya usawa kwa mujibu wa Sheria na taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba, isiyoongozwa kwa misingi ya kidini, yenye watu wenye dini na imani tofauti.

Tunatambua pia kuwa Sheria zetu zimeweka haki ya Uhuru wa kuabudu (Ibara ya 19 (1), (2) na (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1977) na haki ya kutobaguliwa kwa misingi yoyote ile (Ibara ya 13 (4) na (5) ya Katiba hiyo hiyo). Vile vile tunao ufahamu juu ya wajibu wa kuheshimu na kuthamini imani za watu wengine zitokanazo na uvumilivu wa kiimani, na tunatambua kuwa chini ya Sheria ya kanuni ya adhabu (Kifu. 129) Sura ya 16 ya marekebisho ya mwaka 2002 ni jinai kwa mtu yeyote kukashifu ama kuumiza hisia za dini ya mtu mwingine. Tunafahamu kuwa haki hizi zinatekelezwa kwa usimamizi wa mkono wa Serikali na Mamlaka za dola ya Nchi kama ilivyoainishwa katika ibara ya 30 ya Katiba yetu (imetajwa hapo juu). Haya yote yanatufanya tuamini na kutambua kuwa tunaishi katika Nchi yenye Mamlaka zinazofuata Utawala wa Sheria, haki na usawa kwa watu wote.

UTAMBULISHO:

Ifahamike kuwa Umoja wetu kama ilivyo kwa makundi mengine ya kijamii umetambulika kisheria kwani umesajiliwa. Namba ya usajili ni NO/NDC/VUM/166/ ya tarehe 24/06/2011 na shughuli zetu miongoni mwa zingine, ni kuwaongoza Wakristo kwa ujumla wao bila mipaka ya Madhehebu yao, katika mafundisho juu ya dini yao na ukweli kuhusu Mungu na miungu wengine kwa mujibu wa Imani ya Kikristo. Tunafahamu kuwa kwa kufanya hivi hatuvunji Sheria ya Nchi wala taratibu zilizowekwa maana ndivyo hata Katiba yetu iliyosajiliwa inavyoeleza. “Ibara ya 19 (2) kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi, na shughuli ya uendeshaji wa Jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya Nchi”

MASIKITIKO YETU:

Pamoja na yote yaliyoelezwa hapo juu, tunasikitika kueleza matukio yanayoashiria kupoa kwa ushirikiano kati ya Serikali ama Mamlaka zake hapa Wilayani dhidi ya Kanisa (Wakristo). Matukio haya yamevumiliwa na Kanisa tangu Mkuu wa Wilaya ashike madaraka katika Wilaya hii. Kwa Neema na kuchukuliana ambako Mungu wetu ametuagiza, tunayaeleza baadhi ya matukio hayo hapa kama ifuatavyo:

Tamko la kutotambua Umoja wetu.

Mkuu wa Wilaya yetu ya Nzega alitutamkia tarehe 20/02/2013 kwamba hautambui Umoja wetu wa Madhehebu ya Kikristo hapa Nzega. Tunasikitika kupokea kauli ya namna hii kutoka kwa kiongozi wa kitaifa kwa kikundi cha kidini, tena kilichosajiliwa na kinachoendesha shughuli zake kihalali kwa mujibu wa Sheria. Usajili wetu ni kama ulivyoelezwa hapo juu na ofisi ya Wilaya inazo nyaraka zetu na uongozi wetu (Rejea UTHIBITISHO NO. NDC/VUM/166 YA TAR. 24/06/2011).

Mapokezi duni ya Balozi wa Vatican hapa Tanzania alipokuwa hapa Nzega.

Tarehe 24/01/2013 balozi wa Papa (wa Vatican) alivyowasili hapa Nzega na alikuwa na Ziara ambayo ilimfikisha Mkoani Tabora Tunatambua kuwa huyu ni balozi wa amani hapa Nchini lakini pia, anayo heshima ya kiseriikali kama ambayo alipewa katika Wilaya zote alipokuwa akipita. Hivi ni kama mapokezi na ulinzi toka Serikalini ngazi ya Wilaya alizokuwa anatembelea Kanisa la Katoliki. Masikitiko yetu ni kuwa alipofika Nzega hakupewa ushirikiano toka ofisi ya Wilaya ikiwa ni pamoja na kunyimwa ulinzi mpaka amri ilipotoka kwa RPC, na kukataliwa kusaini kitabu cha Wageni cha ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nzega. Iweje Wakuu wa Wilaya zingine walizingatia heshima ya balozi wa Vatican isipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Nzega?.

Kuonyesha upendeleo dhahiri ama wa taathira baina ya Makundi ya kidini.

Tarehe 01 – 14/02/2013 Jumuiya ya Waislamu waliendesha muhadhara walipofika hapa Nzega kwa kibali cha Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nzega. Miongoni mwa mafundisho yao ilikuwa ni kuchambua dini mbili yaani Ukristo na Wislamu, kwa kutumia vitabu viwili yaani Biblia na Qoran. Kutokana na matamshi ya mhadhara wao yaliyoashiria uchochezi wa kashfa na matusi dhidi ya ukristo na uislamu na waumini wao, tarehe 08/02/2013 Umoja wa Madhehebu uliiandikia ofisi ya Mkuu wa Polisi (OCD) Wilaya ya Nzega juu ya malalamiko ya lugha ya Kashfa na matusi dhidi ya Ukristo yaliyokuwa yakitolewa na Ustaadh Sheik Mazinge na wenzake.

Baada ya barua hii Mamlaka za Wilaya hazikuchukua hatua yoyote kwa ajili ya amani dhidi yao, na sisi kama Kanisa hatukujibiwa lolote bali tulipokea maelezo tu “ hiyo ndiyo imani yao waislam wanavyoamini hakuna kosa kwao kueleza misingi ya imani yao,” sisi tulivumilia kwa maelezo ya maamuzi hayo pamoja na kwamba waislam walipotosha mafundisho kwa waumini wetu na kuwachanganya juu ya ukweli wa imani yao ya kikristo. Tukaomba Roho wa Mungu, tutambue namna ya kuwaelewesha waumini wetu juu ya usahihi wa imani yetu ya Kikristo. Mhadhara wao uliendelea kwa siku 14 bila kubugudhiwa mpaka ukamalizika salama bila tetesi zozote kwamba kuna uvunjifu wa amani zilizomfikia Mkuu wa Wilaya.


Tarehe 16/02/2013 Umoja wa Madhehebu ya Kikristo Nzega, tuliomba kibali cha Mkutano wa siku 12 (20/02 – 03/03/2013 katika viwanja vya Parking Nzega kwa ajili ya kufundisha kwa usahihi na ukweli na misingi ya Kikristo kwa mujibu wa vitabu vya Mungu (Biblia na Qoran). Tulipewa kibali na Mkuu wa Polisi Wilaya kwa barua ya kumb. Na.NZ/B.3/VOL.V/168 toka Jeshi la Polisi Nzega. Siku mbili baada ya Mkuu wa Wilaya kufungua Mkutano wetu tulipewa agizo kwa maneno bila barua yoyote na yeye mwenyewe kuufunga Mkutano kwa madai kuwa kuna taarifa za uvunjifu wa amani, na yeye kama Mkuu na Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama akachukua hatua ya kuufunga Mkutano wetu.

Kanisa halikuona sababu ya kufungwa kwa Mkutano huo, ndipo palipokuwa na majadiliano ya tarehe 22 – 23 /02/2013 pamoja na Kamati ya ulinzi na usalama, ikajulikana kuwa sababu ati ilikuwa ni kutumika kwa vitabu viwili yaani Biblia na Qoran, kisha tukaruhusiwa kuendelea na Mkutano kwa masharti ya kulinda imani za wengine kutozitaja dini za wengine. Haya tuliyazingatia kwa kuendelea kufundisha usahihi wa imani ya Kikristo kwa mujibu wa vitabu vya Biblia na Qoran. Siku mbili kabla ya tamati ya Mkutano wetu, tuliamrishwa tena kufunga kutano letu kwa madai ya kuwa ati tumekiuka makubaliano ya kulinda imani za watu wengine. Kwa vile tulifundisha mada Mohamad utume kapewa na nani?. Kitu tunachojiuliza ni kwamba iweje iwepo sheria ya kuruhusu waislam kutumia vitabu viwili yaani Biblia na Qoran bila tatizo, wala masharti kama tuliyopewa Kanisa, lakini iwe tatiza kwa wakristo je, huu sio Ubaguzi ulikatazwa,

Ibara ya 13 (5). “Kwa madhumuni ya ufafanuzi wa ibara hii neno “Kubagua” maana yake ni kutimiza haja, haki au mahitaji mengineyo kwa watu mbalimbali kwa kuzingatia utaifa wao, kabila, pa hala walipotokea, maoni yao ya kisiasa, rangi, dini, jinsia au hali yao ya maisha kwa namna ambayo watu wa aina Fulani wanafanywa au kuhesabiwa kuwa dhaifu au duni na kuwekewa vikwazo au masharti ya vipingamizi ambapo watu wa aina nyingine wanatendewa tofauti au wanapewa fursa au faida iliyoko nje au sifa za lazima.”

Na je kutuzuia kutumia vitabu vya Biblia na Qoran si kutunyima haki ya kueneza imani yetu kwa usahihi kama vile tunavyoamini. Maana kama vile waislam waaminivyo mambo ambayo hayakubaliani na imani yetu, hivyo hivyo na sisi tuaminivyo hata kama hatukubaliwi na imani zingine, tunayo haki ya kueleza, kufundisha, kutetea imani yetu kama walivyo watu wengine. Sote tunaelewa kabisa kwamba mahubiri ama mafundisho ya waislam kwa sehemu kubwa ni makufuru na/au matusi kwa wakristo na Mungu wao. Lakini kwa vile Katiba ya Nchi inalinda haki ya misingi ya uhuru wa kuabudu ambayo mhimili wake ni kuvumiliana kiimani, yaani religious tolerance, sisi wakristo tunawavumilia waislam na kuwapenda, kwa vile ndiyo imani yao ambayo Kikatiba ni haki yao kuishikiria. Vivyo hivyo ikiwa waislam wanaona mahubiri na mafundishao ya wakristo ni makufuru au matusi kwa dini yao, wazingatie kwamba na sisi ndiyo imani yetu, hivyo wajibu wao kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Nchi ni kuvumiliana kama sisi tunavyopaswa kuwavumilia wao.


Kushindwa kwa Serikali na Mamlaka ya Wilaya kulinda Wakristo wakati wa Ibada zetu.


Mikutano kama ule wa tarehe 20/2 – 3/3/2013 ambao ulisitishwa kama ilivyoelezwa hapo juu ni Ibada katika imani yetu ya Kikristo. Ibara ya 13 (1) ya Katiba yetu inaagiza usawa na haki ya kulindwa watu wote bila upendeleo, inayosema “Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wenye haki, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.” bila ya ubaguzi wowote, ndiyo maana majeshi kama Polisi yapo kwa ajili hii. Tunashangazwa na Jambo la kuufunga Mkutano wetu (ambao kwetu ni ibada) kwa sababu kuwa ati kuna watu wamejipanga kuvuruga amani. Sisi kama Watanzani tunahaki ya kupatiwa ulinzi kutoka Jeshi la Polisi lenye dhamana ya ulinzi wa raia wa mali zao. Iweje badala ya kuja kutulinda dhidi ya wale wanaodhaniwa kuja kutuvurugia amani tuamrishwe kufunga Mkutano?. Huku ni kutuvurugia ibada na kumdharau dhahiri Mungu tunayemwabudu Wakristo, kwa Serikali kushindwa kutumia vema mamlaka ya dola kwa Kutulinda.

Kufanya maamuzi kwa tetesi zisizothibitika.



Habari juu ya dalili za kukosekana kwa amani katika Mkutano wetu zilifikishwa ofisi ya Mkuu wa Wilaya tarehe 21/02/2013 na Katibu wa CCM wa Wilaya ya Nzega (kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya). Hazikuwa kwa barua kama tulivyolalamika sisi wakati wa mhadhara wa waislamu kwa maana hiyo tunaamini kuwa haikuwa kiofisi, wala rasmi, maana ofisi ya Wilaya haifanyi kazi kwa mazungumzo ya kijiweni. Habari hizi hata hivyo hazikufanyiwa utafiti wa kii - ntelijensia kufahamu ukweli wake juu ya ni nani? wanataka kufanya nini? na wanasababu zipi?. Na Je sababu hizo ni sahihi ama sivyo. Kwa kitendo hiki Serikali haikututendea haki sisi kama “Kanisa.”





Kuingilia Uhuru wetu wa kuabudu pasipo sababu za msingi.



Tunatambua kuwa Sheria inaruhusu mamlaka za dola na Serikali kuingilia haki za raia ili kulinda maslahi mbalimbali ya watu wengine ama Taifa na Umma kwa ujumla (Ibara ya 30 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977). Pia tunafahamu kuwa Ibara ya 13 (2) inazuia kuweka sharti lolote litakaloonyesha ubaguzi wa dhahiri ama taathira yake. “Inayosema ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake.” Kitendo cha mamlaka za Wilaya chini ya Mkuu wa Wilaya kuvunja ibada yetu katika Mkutano wa tarehe 02/03/2013 kwa sharti la kukiuka makubaliano ama kutumia kitabu cha dini nyingine (Qoran) ni kutumia Sharti la kibaguzi wa dini uliyomo ndani yake na kuonyesha kuwa dini ya uislam ni bora na inasitahiri kutumia Biblia, lakini siyo dini ya ukristo na haisitahiri kutumia Qoran, kwani wakati wa mhadhara wa Waislamu wa kati ya tarehe 01- 14/02/2013 wao pia walitumia vitabu vyote viwili bila ya kizuizi na sharti lolote, licha ya sisi kama Wakristo kuandika barua ya kulalamika dhidi ya kashfa na matusi juu Ukristo na viongozi wake ya tarehe 08/02/2013 bila Serikali kujibu wala kuchukua hatua yoyote ili kulinda Amani.



Pia tunaomba ifahamike kuwa kazi ya kutangaza na kueneza dini na namna yake iko mikonono mwa dini zenyewe na siyo Serikali kwa mujibu wa ibara ya 19 (2) Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977. “Ibara ya 19 (2) kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi, na shughuli ya uendeshaji wa Jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya Nchi.”



Hivyo kuingilia utaratibu na kutuelekeza namna ya kufundisha mafundisho yetu ni kinyume cha Sheria na pia ni matumizi mabaya ya mamlaka ya Umma. Hii ni uchochezi dhahiri na kutugombanisha dhidi ya dini hizi mbili yaani ukristo na uislam (Kutuundia uadui).





Ushirikiano usio sawa kati yetu kama Jamii, ishara ya Ubaguzi.



Mkuu wa Wilaya ya Nzega kama mamlaka Kuu ya dola Wilayani anategemewa kwa kiasi kikubwa kuonyesha ushirikiano wa karibu na wa usawa na makundi yote halali ya kijamii kwa ajili ya ustawi wa jamii yetu.

Upo uthibitisho kuwa Mkuu wa Wilaya wetu alipofika kuongoza Wilaya yetu mapema mwaka 2012 uongozi wa Kanisa ulimfuata ofisini kwake na kumuomba akutane na viongozi wa Kanisa, yeye alitamka kuwa hatambui Umoja wa Madhehebu ya Kikristo ambao ndiyo unakusanya makundi ya CCT, TEC NA PCT hapa Wilayani Nzega. Je, sio dharau dhahiri ya kuvunja Umoja wetu na kufanya sera ya mkoloni Mwingereza ya “divide and rule”?. Cha kushangaza wakati Fulani hata gari yake ya kazi ya Mkuu wa Wilaya (DC) imetumika kumfuta Sheikh wa Wilaya kama kiongozi wa dini ya kiislam (Gari iliyonunuliwa kwa ushuru wa wananchi wa dini zote na wasio na dini) pale alipochelewa futari ya mfungo wa Ramadhani iliyopita ambayo iliyoandaliwa na DC mwenyewe. Je, viongozi na dini zingine wana hadhi tofauti kwa kiongozi wetu yaani Mkuu wa Wilaya kiasi kwamba wakati viongozi wengine na umoja wao hawatambuliwi, wakati wengine wananafasi hata ya kutumia gari lake la kazi?





HITIMISHO: TAMKO RASMI.





Sisi kama Jumuiya ya kidini inayounganisha wakristo wote Wilaya ya Nzega, tunaiheshimu sana Serikali yetu, maana ni mamlaka ambayo Mungu ameipa kibali cha kutuongoza kwa hekima. Tunaheshimu haki na uhuru wa watu wengine kuabudu na kufanya shughuli zao tofauti kwa amani. Pia tunaheshimu Utawala wa Sheria ambao ndiyo msingi wa Umoja wa Taifa letu, lakini kwa sababu ya vitendo hivi vilivyotajwa humu vya Serikali na mamlaka zake Wilayani kwetu hapa hivi karibuni, hasa dhidi yetu kama Kanisa tunatamka kama ifuatavyo:-



Tumekosa imani na Serikali na Chama kinachounda Serikali na mamlaka zake Wilayani kwetu. Kwa kuwa Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa mujibu wa kauli na madai ya Mkuu wa Wilaya ndiye alianza kupeleka habari za uvunjifu wa Amani hata Mkuu wa Wilaya kusikitishwa sana wakati haikuwa hivyo.



Tumesitisha ushirikiano na Serikali ya Wilaya, kwa kutokuwa na Imani na viongozi wa Serikali ya Wilaya (Mkuu wa Wilaya), na Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Ni kwa kutokana na kikao cha viongozi wa Umoja wa Madhehebu ya Kikristo tarehe 07/03/2013, tunatoa taarifa kwa waumini wote wa Kikristo Wilayani, Mkoani na Nchi nzima na ngazi za juu zaidi za Serikali na mamlaka za dola ili watambue kwamba tunaishi chini ya kifungo kisicho dhahiri lakini kilicho wazi kwa tafsiri yake.























0 comments:

 
Powered by Blogger