Translate

Sunday, May 12, 2013

KWA NINI NAUNGA MKONO KAULI YA WAZIRI NCHIMBI KUHUSU KUSIMAMISHWA MIHADHARA

Kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Emmanuel Nchimbi, inapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania mwenye mapenzi mema.

Mihadhara ilipoanzishwa mwaka 1985 ilijikita zaidi kwenye masuala ya imani tu kwa maana ya kulinganisha vitabu yaani Qur'an na Biblia.

Kwa wale wasiofahamu ndani ya Qur'an kuna aya 62 zinazowataja Wakristo  na imani yao.

 Mihadhara au midahalo ilifanyika tangu kipindi Mtume Mohammad s.a.w akiwa hai. Mfano ni pale alipofanya mdahalo na Wakristo wa Najran walipokuwa wakijadili hoja kuhusu fundisho la Uwana wa Mungu. Hata hivyo walimaliza kwa amani kwa kukubaliana kutokukubaliana.

Kwa karne karibu 14 suala hilo limekuwepo katika ngazi mbali mbali za kiimani.

Hata hivyo, huku kukiwepo  na mihadhara hiyo, mwaka 2010 katika hali ya ghafla sana na bila matarajio, kulizuka kundi lililokuwa likitaka ufuatwe tu msingi wa kidini bila kuangalia mazingira yake.

Kibaya zaidi kundi hilo likaanza hata kuwashambulia wafuasi wa dini ya Kiislamu sanjari na Wakristo, huku likiwashutumu Waislamu wenye mapenzi mema kwa kushirikiana na wale wasio Waislamu, yaani Wakristo. Hali ikazidi kuwa tete baada ya kuanza kuwadhuru viongozi wa dini hizo zote .

Hata hivyo kundi hilo si la wale wanaofanya mihadhara, bali lilitaka kufanya kama vile walivyokuwa wakifanya waliokuwa wakifanya mihadhara. Kwa mtu asiyejua hawezi akajua tofauti yake.

Kibaya zaidi waandaaji wa mikakati hiyo (thinking tank) si wale wanaoonekana wakihutubia hadharani,  bali huitayarisha kisha kuwapatia hao wanaoonekana wakihutubia au kutishia.

 Utafiti wangu wa miaka mitatu sasa, umegundua kuwa hao waandaaji wa harakati hizo, ni watu wanaoheshimika katika jamii, wengine ni wanasiasa, wengine wanataaluma wakubwa, na wafanya biashara.
Lengo kuu ni kutengeneza himaya itakayokuwa na maamuzi ya mwisho katika mambo mengi ya kijamii, kiuchumi na kisiasa (religious preference).

Wengine ni watumishi wa Umma na unapojaribu kuwagusa kwenye hili, unakuwa umetangaza vita ambayo jamii haitajua chanzo cha vita hiyo isipokuwa mhanga na huyo aliyeguswa. Majina yao yanafahamika na hata jamii ikitajiwa inaweza kushangaa. Lakini wapo.

Kwa  sababu yako mambo mengine ambayo unapoyasikiliza yanapotamkwa kwa haraka unagundua kwamba ujumbe ule yuko aliyeuandaa kwa manufaa ya kundi husika na siyo mtamkaji.

Kwa muono wangu, hata kama wangekamatwa wanaotamka bila kupatikana waandaaji bado haitasaidia sana kuleta utulivu kwa sababu waandaaji hao, wanaweza kumtafuta mtu mwingine wakampa ujumbe wao huo.

Kwa hiyo, kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani kufungia mihadhara iwe hatua ya kwanza tu, lakini pia kuanza kufuatilia wanaopanga mikakati hiyo, iwe hatua ya pili.

Kwa wale waliokuwa wakijaribu kufafanua kwa njia ya kujibu, ilikuwa ni kwa sababu hakukuwepo na kauli kama hii ya Serikali, kwa hiyo kwao walikuwa wanajitetea wenyewe kwa njia ya kujibu shutuma.

Hii ndiyo sababu naiunga mkono kauli ya Waziri Nchimbi. 

TANZANIA KWANZA!!!

0 comments:

 
Powered by Blogger