Translate

Thursday, December 5, 2013

TETESI ZA KUVUNJWA MISIKITI ANGOLA: FUNZO KWA WAPENDA AMANI TANZANIA

Tetesi za hivi karibuni katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ya kupigwa marufuku kwa dini ya Kiislamu katika nchi ya Angola zinatushtua sana, hasa kwa sisi wapenda amani.

 Tetesi zinadai kwamba, Uislamu unapigwa marufuku kwa sababu, Waangola hawataki siasa kali za kidini katika nchi yao. Huenda ni kwa sababu wanajua athari zake kwa sababu walionja athari za vita. Marufuku hiyo wanadai inaambatana na uvunjwaji wa misikiti. Hili nalo linatisha zaidi halijawahi kutokea. Hata hivyo, jumuia ya Kiislamu ya O.I.C imeziomba jumuia za kimataifa kuingilia kati suala hilo kwa kuionya Angola isitekeleze mpango huo kwa sababu unavunja haki za binadamu za uhuru wa kuabudu. Na mimi naupinga mpango huo.

Hata hivyo tukio hili ikiwa ni la kweli au sivyo, linapaswa lichukuliwe kuwa ni funzo moja kubwa sana kwa wafuasi wa dini mbali mbali. Kwamba kumbe unapohujumu mambo ya dini ya mwenzako ikiwemo kuchomwa na kuvunja makanisa, ni lazima ujue unaumiza sana hisia za wafuasi wa dini husika, hata kama utawaona wamekaa kimya bila kujibu lolote, lakini kihisia wanakuwa wameumia sana sana. 

Ikiwa ndivyo hivyo je tuko tayari kulaani hata ikibidi kuwataja wafuasi wa dini zetu ambao tunawajua wako mstari wa mbele kubomoa, kuchoma na hata kuua au kumwagia tindikali viongozi wa dini tofauti na yetu tunayoiamini? Ikiwa tetesi tu za kubomolewa misikiti 80 Angola zimemfanya Mufti wa Misri kuchukia na kuiomba jumuia ya Kiislamu Duniani (O.I.C) kuingilia kati, je unafikiri kuchomwa makanisa, kubomolewa na kuuwawa viongozi wa dini ya Kikristo, ndugu zao Wakristo wa sehemu nyingine duniani hawaumii kihisia? Au unapommwagia tindikali Sheikh au Imam wa msikiti unajenga amani au unaibomoa? Kufanya hivyo unaumiza hisia za wafuasi wao.

Iwapo tetesi tu za kupigwa marufuku Uislamu Angola ziliibua hisia za wafuasi wa dini hiyo ulimwenguni, je unafikiri inakuwaje kwa wafuasi wa dini inayohujumiwa? 

Tunayo mambo mengi ya kujifunza kupitia tetesi hizo ili tujitahidi kujiepusha na viashirio vyovyote vinavyoweza kutuondolea tunu za amani tulizo nazo Watanzania.Tunapo pa kuanzia-Angola. Wewe unasemaje?

0 comments:

 
Powered by Blogger