Translate

Tuesday, June 18, 2013

KIKWAZO CHA KIIMANI KWENYE RASIMU YA KATIBA MPYA TANZANIAIbara inayohusiana na uhuru wa kuabudu, ina utata mkubwa. Utata huu, unasababishwa na upungufu wa tafsiri. Utata huo utazua  mtafaruku mkubwa baina ya makundi ya kiimani na vyombo vya dola, pale vyombo hivyo vitakapokuwa vikiingilia  taratibu za dini hizo kwa kuzitafsiri kuwa ni kashfa.

Ibara hiyo inasomeka hivi: 31.-(5) Ni marufuku kwa mtu, kikundi au taasisi ya dini kutumia uhuru
wa kutangaza dini kwa kukashifu imani na dini nyingine, kujenga chuki au
kuchochea vurugu na ghasia kwa madai ya kutetea imani au dini.

Vyombo vya kutafsiri sheria, vimekuwa vikipata ugumu wa kupata tafsiri sahihi kuhusiana na neno kashfa, au kwamba ni kitendo gani kinapofanyika huhesabika kuwa mtu ametenda kosa la kukashifu.

Neno kashfa lina asili yake kutoka katika lugha ya Kiarabu.Maana yake funua kilichofunikwa.

Katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania  uk.147  neno kashfa limetafsiriwa kuwa ni :- "ufunuaji au udhihirisho wa jambo la aibu;  na Kashifu ni:- kutoa nje siri ya jambo la aibu; nyambua 2. jua au fahamu jambo la siri la moyoni mwa mtu mwingine kabla mwenyewe hajalieleza."

Maana ya wazi zaidi ni mfano wa mtu mume anapofunua maungo ya mwanamke asiye mke wake. Tendo hilo ndilo linalokamilisha tendo la kashifa kwa maana ya kufunua jambo la aibu.

Tendo la kusema kinyume na imani ya dini linaitwa kukufuru na wala siyo kukashifu. Neno kufuru halimo katika rasimu ya Katiba hii.

Kamusi ya Kiswahili Sanifu uk.137 inatafsiri neno kufuru ambalo ni kitenzi na la kidini kuwa ni:- sema jambo ambalo ni kinyume na imani ya dini 2. kataa kufuata imani ya dini baada ya kuhubiriwa.

Lakini neno kufuru linapokuwa jina lina maana ya:- tamko  au maneno ambayo ni kinyume na imani ya dini. 2. dharau dini

Hili litaleta changamoto kubwa katika imani zetu. Kwa mfano baadhi ya vitabu vya dini vinataja kwa uwazi habari za watu wa dini zingine. Mfano Qur'an Tukufu inataja habari za Wakristo mara 62.

 Moja ya aya hizo ni ile iliyomo ndani ya Qur'an, Suratul Al-Maidah, 5:14 inasema: "Na kwa wale waliosema: "Sisi ni Wakristo," tulichukua ahadi kwao, lakini wakaacha sehemu (kubwa)" ya yale waliyokumbushwa, kwa hivyo tukaweka baina yao (wenyewe kwa wenyewe) uadui na bughudha mpaka siku ya Kiyama. Na Mwenyezi Mungu atawaambia waliyokuwa wakiyafanya." (tafsiri ya Sheikh Abdullah Saleh al-Farsy)

Ikiwa neno Kashfa litatafsiriwa kuwa ni uchochezi, itabidi aya hizo 62 zilizomo ndani ya Qur'an zifutwe ili kuwaepusha Waislamu kuingia katika hatia hiyo itakayowasababishia vifungo magerezani.

Lakini pia neno kashfa hata sasa limeendelea kuleta utata hata katika mahakama zetu ambazo, mara nyingi hushindwa kupata tafsiri sahihi kuhusiana na neno hilo

Pia itabidi kila Muislamu anaposoma aya za Qur'an anapofikia aya zile zinazotaja watu wa dini nyingine mfano Wakristo na Wayahudi, aziruke aya hizo ili kuepuka kufungwa.


Upande wa Waislamu waliwahi Sheikh Abu Aziz alimwandikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali waraka  wa tarehe 15 Mei, 1998 ambao walikuwa wakielezea utetezi wao kuhusiana na neno kashfa , baada ya kutuhumiwa kwamba katika mahubiri yao wanatoa kashfa. Walisema, ninanukuu:


("Definition") maelezo bayana ya kashifa 
"Concise Oxford) English Dictionary" inaielezea kashfa/kufuru (blasphemy) kuwa ni kusema kwa kutoyaheshimu mambo matakatifu; kusema kukufuru kuhusu jambo; kutusi, kwa mujibu wa "Osbern law Dictionary" kashfa/kufuru ni kusema kwa kukejeli hadharani au kwa makosa ya jinai juu ya mambo yanayomuhusu Mungu, Yesu Kristo, Biblia .... kwa dhamira ya kuleta dharau na chuki dhidi ya Kanisa kwa mujibu wa sheria zilizopo. 

Kwa jumla kufuru/kashfa inaelezeka kuwa ni pale yanaposemwa mabaya juu ya Mungu kwa lengo la kukejeli ili kushusha hadhi ya utukufu wa Mwenyezi Mungu na kuyaondoa mawazo ya watu kwenye kumcha na kumpenda Mungu. Ni kutumia maneno juu ya Mwenyezi Mungu makusudi kwa dhamiri na mpango wa kuzuia na kuvunja heshima, unyenyekevu na imani anayoistahiki kama Muumba, mjuzi wa kila kitu, mtawala na mhukumu wa dunia. Inaleta dhana ya kupuuza, inapotumika juu ya Mungu, kama vile dharau mara kwa mara inavyokuwa na dhana hiyo pale inapotumiwa juu ya mtu binafsi. Ni kwa makusudi na kwa nia mbaya kujaribu kumuondolea mwanaadamu unyenyekevu wake kwa Mola wake kwa kukana kuwepo kwake, au sifa zake kama Muumba mjuzi wa kila kitu, mtawala na anayehukumu watu wote na kuwazuia watu wasiwe na imani naye. 

Lazima kutofautisha baina ya kashafa/kufuru na uzurishi (heresy), ambayo "Osborn Law Dictionary" inaielezea kuwa ni kosa la kanuni za kidini linalotokana na mtu kuwa na mawazo ya uongo yanayochukiza na yasiyokubalika kwa kuhalifu nguzo mojawapo ya imani ya Kikristo. 
Kushambulia "kweli" ya Ukristo si kosa kwa mujibu wa common law. 

"Digest of Criminal Law" (9th edition) ya Stephen inasema sheria ya kashfa/kufuru kwa mujibu wa "common law" iko kama ifuatavyo: "Kila andiko linahesabika kuwa ni kashfa pale linapokuwa na jambo lolote ambalo linadharau, linatukana au linakejeli Mungu, Yesu kristo au Biblia au Kanuni za Kanisa la Uingereza kama ilivyowekwa na sheria. Si kashfa kusema au kuandika na kutoa mawazo ambayo yanapingana na dini ya Kikristo, au kukana kuwapo kwa Mungu, kama matamshi/maandishi yenyewe yanayotolewa kwa lugha yenye heshima na iliyo ya kistaarabu. Kipimo cha kutumia ni kutazama namna ya jinsi itikadi zenyewe zinavyoelezewa na siyo juu ya kile kilichomo ndani ya itikadi hizo" (msisitizo unaongezwa). 

Katika kesi baina ya Bowman dhidi ya Secular Society (1917) Bunge la juu la Uingereza (House of Lords) liliamua kuwa kuishambulia au kuikana kweli ya Ukristo, bila ya kutia matusi, kejeli au utovu wa hesima juu ya mambo matakatifu, si kuvunja sheria. Na kwenye kesi baina ya R na Lemon (1979) ambapo wachapishaji wa gazeti la "Gay News" walipitisha shutuma za kashfa zilizokuwa na maneno yaliyodhaniwa kukasirisha na kutukana hisia za mkristo (kiasi ninavyomuheshimu na kumpenda Bwana Yesu (AS) siwezi kuyarudia yale yaliyosemwa. Mahakama ya Rufaa iliamua kuwa kauli inaweza kuwa ya kashfa kama hoja yake imekuwa ya kuumiza na kutukana; ikijiegemeza siyo kwenye matumizi ya akili, bali kwenye hisia za kinyama na zisizo za kuungana na maumbile ya mwanadamu. Baadaye kwenye kesi hiyo hiyo Bunge la juu ya Uingereza likasisitiza kuwa, katika mashauri ya kashfa, kipimo kimo katika uwezekana wa kukasirisha na kutukana na siyo uwezekano wa kuvunjika kwa amani. 

Kwa hiyo inajulikana na kukubalika kuwa kwa mujibu wa common law si kashfa kushambulia misingi ya dini kama kanuni za kuweka heshima na uungwana katika malumbano zitafuatwa. Kwa kweli Tume ya Sheria ya Uingereza iliamua mwaka 1985 kuwa common law si chombo kinachofaa kuhakikisha kuwa imani za dini zinaheshimiwa, na kwamba kosa la kashfa chini ya kanuni za common law lifutwe hasa kwa sababu yamewekwa makosa mengine katika sheria yanayoshughulikia mwenendo mbaya unaoingilia ibada za hadhara, au mwenendo wa kutukana wafuasi wa vikundi mbalimbali vya dini ambao unaweza kuletea kuvunjika kwa amani. Inahusika hapa kuzingatia kuwa nchini Uingereza mashitaka dhidi ya makosa ya kashfa yamekuwa machache na kwa kweli kesi ya lemon imekuwa mashitaka ya kwanza baada ya miaka sitini.  


Kuwazuilia watu uhuru wa kuabudu nchini Tanzania
Sheria za makosa ya jinai nchini Tanzania kwa msingi zimechukuliwa kutoka sheria za Waingereza; sehemu kubwa ya Penal Code kutokana na "Draft Code" ya Sir James Fitzjames Stephen ya mwaka 1878. 

Miaka ilivyopita kulifanyika mabadiliko yaliyolazimishwa na matakwa ya hali halisi nchini. Kwa mfano kwenye makosa ya jinai yanayohusiana na uhuru wa dini, sehemu zote zinazomtaja Yesu Kristo, Ukristo na Kanisa la Uingereza, zilifutwa, bila ya shaka kwa sababu ya kutambua kuwa Tanzania, hapo sheria hii ilipowekwa ni nchi ya mchanganyiko wa urithi wa dini nyingi na tamaduni mbalimbali. 

Hali halisi hii haijabadilika; sababu zilizopelekea kuwako kwa hali halisi hii hazijabdilika. Kwa hiyo kifungu cha 129 cha "Penal Code" kinachoainisha makosa ya jinai kwenye uhuru wa dini kama unavyotolewa na kifungu cha 19 cha katiba ya Jamhuri ya Muungano kinaeleza kuwa "Mtu yeyote ambaye, kwa dhamiri za makusudi za kutaka kuumiza hisia za mtu yeyote, anatamka neno lolote, au anatoa sauti yoyote inayosikiwa na mtu huyo, au anatoa ishara yoyote inayoonekana na mtu huyo, atakuwa amefanya kosa." 
Hatia ya kosa la kutamka maneno kwa dhamiri ya kuumiza hisia, inategemea ushahidi kuwa maneno hayo yalitamkwa kwa dhamiri ya kuumiza hisia na kwamba maneno hayo kweli yameumiza hisia. 
 
Nini kashfa nchini Tanzania:  
Kwa hiyo, tukizingatia urithi wetu Tanzania wa kuwa na wananchi wa mchanganyiko wa dini mbalimbali si kosa la jinai kwa ukristo kusema kuwa Yesu ni Mungu au ni mwana wa Mungu, huo ukiwa ndio msingi wa imani ya kikristo. Wala siyo kosa kwa Muisilamu kusema kuwa Yesu si Mungu au Mwana wa Mungu, hii ikiwa nguzo katika imani ya Uisilamu kwamba Mungu ni mmoja tu na hakuna waliosawa naye washirika, au wana. Si kosa vile vile kwa mkristo kusema kuwa Yesu alisulubiwa na akafufuka; hii ikiwa msingi katika Ukristo. Na wala si kosa kwa Muisilamu kusema kuwa Yesu hakusulubiwa wala hakufufuka; hii ikiwa ni sehemu ya imani ya Uisilamu kwamba hakuna kutolewa muhanga kwa ajili ya kufuta dhambi za wengine. La kweli ni kuwa kilicho kufuru kwa Ukristo si kufuru katika Uisilamu na kilicho kufuru kwa Uisilamu si kufuru kwa Ukristo. 


Inatuhusu hapa kuzingatia kuwa kwa mujibu wa Criminal Procedure Act ya 1985, kosa la makusudi kusema maneno yanayodhamiria kuumiza hisia za kidini ni kosa linalohitaji waranti katika kumkamata mkosaji, na waranti unatakiwa utolewe na hakimu pahali pa kazi kufuatia malalamiko, kabla mtu hajakamatwa. Hii maana yake ni kwamba, kwa; maneno mepesi, kabla mtu yeyote hajakamatwa na kushitakiwa kwa kosa la makusudi kusema maneno yaliyodhamiria kuumiza hisia za kidini, kwanza mtu lazima apeleke malalamiko yake na yatiliwe mkazo kwa kiapo kwenye mahakama kabla ya waranti wa kumkamatia mtu haujatolewa. Kwa hiyo ni kwenda kinyume cha sheria kumkamata mtu ambaye hakuna shitaka lililotayarishwa au waranti wa kumkamatia kutolewa. Inafaa kuzingatia kuwa polisi wa Tanzania hawajafuata utaratibu huu hata mara moja katika harakati zao za kuwakamata wahubiri wa Kiisilamu, jambo ambalo linadhihirisha ama kutojua kazi kwao, au hisia zao za udini." mwisho wa kunukuu 
 
Hili litaleta mfarakano mkubwa sana badala ya kuleta utengamano. Tulirekebishe mapema.

0 comments:

 
Powered by Blogger